Zaburi 52
Hukumu Ya Mungu 
Kwa mwimbishaji. Utenzi wa Daudi. Baada ya Doegi, Mwedomu kumwendea Sauli na kumjulisha kuwa: “Daudi amekwenda nyumbani kwa Ahimeleki.” 
 1 Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya? 
Kwa nini unajivuna mchana kutwa, 
wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu? 
 2 Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi. 
Ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila. 
 3 Unapenda mabaya kuliko mema, 
uongo kuliko kusema kweli. 
 4 Unapenda kila neno lenye kudhuru, 
ewe ulimi wenye hila! 
 5 Hakika Mungu atakushusha chini 
kwa maangamizi ya milele: 
atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu 
kutoka hema yako, 
atakungʼoa kutoka nchi ya walio hai. 
 6 Wenye haki wataona na kuogopa, 
watamcheka, wakisema, 
 7 “Huyu ni yule mtu ambaye 
hakumfanya Mungu kuwa ngome yake, 
bali alitumainia wingi wa utajiri wake, 
na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!” 
Neema Ya Mungu 
 8 Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni 
unaostawi katika nyumba ya Mungu, 
nautegemea upendo wa Mungu usiokoma 
milele na milele. 
 9 Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda, 
nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema. 
Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.