Zaburi 53
Uovu Wa Wanadamu 
(Zaburi 14) 
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi. Utenzi wa Daudi. 
 1 Mpumbavu anasema moyoni mwake, 
“Hakuna Mungu.” 
Wameharibika, na njia zao ni za uovu kabisa, 
hakuna hata mmoja atendaye mema. 
 2 Mungu anawachungulia wanadamu chini 
kutoka mbinguni 
aone kama wako wenye akili, 
wowote wanaomtafuta Mungu. 
 3 Kila mmoja amegeukia mbali, 
wameharibika wote pamoja, 
hakuna atendaye mema. 
Naam, hakuna hata mmoja! 
 4 Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza: 
wale ambao huwala watu wangu 
kama watu walavyo mkate, 
hao ambao hawamwiti Mungu? 
 5 Hapo waliingiwa na hofu kuu, 
ambapo hapakuwa cha kutetemesha. 
Mungu alitawanya mifupa ya wale waliokushambulia; 
uliwaaibisha, kwa sababu Mungu aliwadharau. 
 6 Laiti wokovu wa Israeli ungalikuja kutoka Sayuni! 
Wakati Mungu arejeshapo wafungwa wa watu wake, 
Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi!