Zaburi 61
Kuomba Ulinzi 
Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za uimbaji. Zaburi ya Daudi. 
 1 Ee Mungu, sikia kilio changu, 
usikilize maombi yangu. 
 2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita, 
ninaita huku moyo wangu unadhoofika; 
uniongoze kwenye mwamba 
ule ulio juu kuliko mimi. 
 3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu, 
ngome imara dhidi ya adui. 
 4 Natamani kukaa hemani mwako milele, 
na kukimbilia chini ya uvuli wa mbawa zako. 
 5 Ee Mungu, kwa kuwa umesikia nadhiri zangu, 
umenipa urithi wa wale wanaoliogopa jina lako. 
 6 Mwongezee mfalme siku za maisha yake, 
miaka yake kwa vizazi vingi. 
 7 Yeye na atawazwe kwenye kiti cha enzi mbele za Mungu milele; 
amuru upendo wako na uaminifu wako vimlinde. 
 8 Ndipo daima nitaliimbia sifa jina lako 
na kuzitimiza nadhiri zangu siku baada ya siku.