Zaburi 62
Mungu Kimbilio La Pekee 
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi. 
 1 Kwa Mungu peke yake nafsi yangu inapata pumziko; 
wokovu wangu watoka kwake. 
 2 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu; 
yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe. 
 3 Mtamshambulia mtu hata lini? 
Je, ninyi nyote mtamtupa chini, 
ukuta huu ulioinama na uzio huu unaotikisika? 
 4 Walikusudia kikamilifu kumwangusha 
toka mahali pake pa fahari; 
wanafurahia uongo. 
Kwa vinywa vyao hubariki, 
lakini ndani ya mioyo yao hulaani. 
 5 Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake, 
tumaini langu latoka kwake. 
 6 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu; 
ndiye ngome yangu, sitatikisika. 
 7 Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu, 
ndiye mwamba wangu wenye nguvu 
na kimbilio langu. 
 8 Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote, 
miminieni mioyo yenu kwake, 
kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu. 
 9 Binadamu wa ngazi ya chini ni pumzi tu, 
nao wa ngazi ya juu ni uongo tu; 
wakipimwa kwenye mizani, si chochote; 
wote kwa pamoja ni pumzi tu. 
 10 Usitumainie vya udhalimu 
wala usijivune kwa vitu vya wizi; 
ingawa utajiri wako utaongezeka, 
usiviwekee moyo wako. 
 11 Jambo moja Mungu amelisema, 
mambo mawili nimeyasikia: 
kwamba, Ee Mungu, 
wewe una nguvu, 
 12 na kwamba, Ee Bwana, 
wewe ni mwenye upendo. 
Hakika utampa kila mtu thawabu 
kwa kadiri ya alivyotenda.