Zaburi 64
Kuomba Ulinzi Dhidi Ya Maadui 
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. 
 1 Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu, 
uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui. 
 2 Unifiche kutokana na shauri la siri la waovu, 
kutokana na zile kelele za kundi la watenda mabaya. 
 3 Wananoa ndimi zao kama panga 
na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha. 
 4 Hurusha mishale kutoka kwenye mavizio kwa mtu asiye na hatia, 
humrushia ghafula bila woga. 
 5 Kila mmoja humtia moyo mwenzake 
katika mipango mibaya; 
huzungumza juu ya kuficha mitego yao, 
nao husema, “Ni nani ataiona?” 
 6 Hufanya shauri baya la dhuluma na kusema, 
“Tumebuni mpango mkamilifu!” 
Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila. 
 7 Bali Mungu atawapiga kwa mishale, 
nao ghafula wataangushwa. 
 8 Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao 
na kuwaleta kwenye maangamizi; 
wote wawaonao watatikisa vichwa vyao 
kwa dharau. 
 9 Wanadamu wote wataogopa, 
watatangaza kazi za Mungu 
na kutafakari yale aliyoyatenda. 
 10 Wenye haki na wafurahi katika Bwana, 
na wakimbilie kwake; 
wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!