Zaburi 65
Kusifu Na Kushukuru 
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Wimbo. 
 1 Ee Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni; 
kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa. 
 2 Ewe usikiaye maombi, 
kwako wewe watu wote watakuja. 
 3 Tulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi, 
wewe ulisamehe makosa yetu. 
 4 Heri wale uliowachagua 
na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako! 
Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako, 
mema ya Hekalu lako takatifu. 
 5 Unatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki, 
Ee Mungu Mwokozi wetu, 
tumaini la miisho yote ya duniani 
na la bahari zilizo mbali sana, 
 6 uliyeumba milima kwa uwezo wako, 
ukiwa umejivika nguvu, 
 7 uliyenyamazisha dhoruba za bahari, 
ngurumo za mawimbi yake, 
na ghasia za mataifa. 
 8 Wale wanaoishi mbali sana 
wanaogopa maajabu yako, 
kule asubuhi ipambazukiapo 
na kule jioni inakofifilia 
umeziita nyimbo za furaha. 
 9 Waitunza nchi na kuinyeshea, 
waitajirisha kwa wingi. 
Vijito vya Mungu vimejaa maji 
ili kuwapa watu nafaka, 
kwa maana wewe umeviamuru. 
 10 Umeilowesha mifereji yake 
na kusawazisha kingo zake; 
umeilainisha kwa manyunyu 
na kuibariki mimea yake. 
 11 Umeuvika mwaka taji ya baraka, 
magari yako yanafurika kwa wingi. 
 12 Mbuga za majani za jangwani umezineemesha; 
vilima vimevikwa furaha. 
 13 Penye nyanda za malisho pamejaa makundi ya wanyama, 
na mabonde yamepambwa kwa mavuno; 
vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba.