Zaburi 66
Kusifu Mungu Kwa Ajili Ya Wema Wake 
Kwa mwimbishaji. Wimbo. Zaburi. 
 1 Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote! 
 2 Imbeni utukufu wa jina lake; 
mpeni sifa zake kwa utukufu! 
 3 Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako! 
Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba 
adui wananyenyekea mbele zako. 
 4 Dunia yote yakusujudia, 
wanakuimbia wewe sifa, 
wanaliimbia sifa jina lako.” 
 5 Njooni mwone yale Mungu aliyoyatenda, 
mambo ya kutisha aliyoyatenda 
miongoni mwa wanadamu! 
 6 Alifanya bahari kuwa nchi kavu, 
wakapita kati ya maji kwa miguu, 
njooni, tumshangilie. 
 7 Yeye hutawala kwa uwezo wake milele, 
macho yake huangalia mataifa yote: 
waasi wasithubutu kujiinua dhidi yake. 
 8 Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu, 
sauti ya sifa yake isikike, 
 9 ameyahifadhi maisha yetu 
na kuizuia miguu yetu kuteleza. 
 10 Ee Mungu, wewe ulitujaribu, 
ukatusafisha kama fedha. 
 11 Umetuingiza kwenye nyavu 
na umetubebesha mizigo mizito 
migongoni mwetu. 
 12 Uliwaruhusu watu watukalie vichwani, 
tulipita kwenye moto na kwenye maji, 
lakini ulituleta kwenye nchi 
iliyojaa utajiri tele. 
 13 Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa 
na kukutimizia nadhiri zangu: 
 14 nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi 
na nilizotamka kwa kinywa changu 
nilipokuwa katika shida. 
 15 Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono 
na sadaka za kondoo dume, 
nitakutolea mafahali na mbuzi. 
 16 Njooni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu, 
nami niwaambie aliyonitendea. 
 17 Nilimlilia kwa kinywa changu, 
sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu. 
 18 Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu, 
Bwana asingekuwa amenisikiliza; 
 19 lakini hakika Mungu amenisikiliza 
na amesikia sauti yangu katika maombi. 
 20 Sifa apewe Mungu, 
ambaye hakulikataa ombi langu 
wala kunizuilia upendo wake!