Zaburi 67
Mataifa Yahimizwa Kumsifu Mungu 
Kwa mwimbishaji. Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi. Wimbo. 
 1 Mungu aturehemu na kutubariki, 
na kutuangazia nuru za uso wake, 
 2 ili njia zako zijulikane duniani, 
wokovu wako katikati ya mataifa yote. 
 3 Ee Mungu, mataifa na wakusifu, 
mataifa yote na wakusifu. 
 4 Mataifa yote wafurahi na kuimba kwa shangwe, 
kwa kuwa unatawala watu kwa haki 
na kuongoza mataifa ya dunia. 
 5 Ee Mungu, mataifa na wakusifu, 
mataifa yote na wakusifu. 
 6 Ndipo nchi itatoa mazao yake, 
naye Mungu, Mungu wetu, atatubariki. 
 7 Mungu atatubariki 
na miisho yote ya dunia itamcha yeye.