Zaburi 86
Kuomba Msaada 
Maombi ya Daudi. 
 1 Ee Bwana, sikia na unijibu, 
kwa maana mimi ni maskini na mhitaji. 
 2 Linda maisha yangu, kwa maana nimejiweka kwako, 
wewe ni Mungu wangu, 
mwokoe mtumishi wako anayekutumaini. 
 3 Ee Bwana, nihurumie mimi, 
kwa maana ninakuita mchana kutwa. 
 4 Mpe mtumishi wako furaha, 
kwa kuwa kwako wewe, Ee Bwana, 
ninainua nafsi yangu. 
 5 Ee Bwana, wewe ni mwema na mwenye kusamehe, 
umejaa upendo kwa wote wakuitao. 
 6 Ee Bwana, sikia maombi yangu, 
sikiliza kilio changu unihurumie. 
 7 Katika siku ya shida yangu nitakuita, 
kwa maana wewe utanijibu. 
 8 Ee Bwana, katikati ya miungu hakuna kama wewe, 
hakuna matendo ya kulinganishwa na yako. 
 9 Ee Bwana, mataifa yote uliyoyafanya 
yatakuja na kuabudu mbele zako; 
wataliletea utukufu jina lako. 
 10 Kwa maana wewe ni mkuu, na unafanya mambo ya ajabu; 
wewe peke yako ndiwe Mungu. 
 11 Ee Bwana, nifundishe njia yako, 
nami nitakwenda katika kweli yako; 
nipe moyo usiositasita, 
ili niweze kulicha jina lako. 
 12 Ee Bwana wangu, nitakusifu kwa moyo wote; 
nitaliadhimisha jina lako milele. 
 13 Kwa maana upendo wako ni mkuu kwangu; 
umeniokoa kutoka kwenye vilindi vya kaburi.* Yaani Kuzimu. 
 14 Ee Mungu, wenye majivuno wananishambulia; 
kundi la watu wakatili linatafuta uhai wangu: 
watu wasiokuheshimu wewe. 
 15 Lakini wewe, Ee Bwana, ni Mungu wa huruma na neema, 
si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo na uaminifu. 
 16 Nigeukie na unihurumie; 
mpe mtumishi wako nguvu zako, 
mwokoe mwana wa mtumishi wako wa kike.† Au: mwokoe mwanao mwaminifu. 
 17 Nipe ishara ya wema wako, 
ili adui zangu waione nao waaibishwe, 
kwa kuwa wewe, Ee Bwana, 
umenisaidia na kunifariji.