Zaburi 98
Mungu Mtawala Wa Dunia 
Zaburi. 
 1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya, 
kwa maana ametenda mambo ya ajabu; 
kitanga chake cha kuume na mkono wake mtakatifu 
umemfanyia wokovu. 
 2  Bwana ameufanya wokovu wake ujulikane 
na amedhihirisha haki yake kwa mataifa. 
 3 Ameukumbuka upendo wake 
na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli; 
miisho yote ya dunia imeuona 
wokovu wa Mungu wetu. 
 4 Mpigieni Bwana kelele za shangwe, dunia yote, 
ipaze sauti kwa nyimbo za shangwe na vinanda; 
 5 mwimbieni Bwana kwa kinubi, 
kwa kinubi na sauti za kuimba, 
 6 kwa tarumbeta na mvumo wa baragumu za pembe za kondoo dume: 
shangilieni kwa furaha mbele za Bwana, aliye Mfalme. 
 7 Bahari na ivume na kila kiliomo ndani yake, 
dunia na wote wakaao ndani yake. 
 8 Mito na ipige makofi, 
milima na iimbe pamoja kwa furaha, 
 9 vyote na viimbe mbele za Bwana, 
kwa maana yuaja kuhukumu dunia. 
Atahukumu dunia kwa haki 
na mataifa kwa haki.