Zaburi 99
Mungu Mfalme Mkuu 
 1  Bwana anatawala, 
mataifa na yatetemeke; 
anakalia kiti cha enzi katikati ya makerubi, 
dunia na itikisike. 
 2  Bwana ni mkuu katika Sayuni; 
ametukuzwa juu ya mataifa yote. 
 3 Wanalisifu jina lako ambalo ni kuu na la kuogopwa: 
yeye ni mtakatifu! 
 4 Mfalme ni mwenye nguvu na hupenda haki, 
wewe umethibitisha adili; 
katika Yakobo umefanya 
yaliyo haki na sawa. 
 5 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu, 
na mkaabudu katika mahali pa kuwekea miguu yake; 
yeye ni mtakatifu. 
 6 Mose na Aroni walikuwa miongoni mwa makuhani wake, 
Samweli alikuwa miongoni mwa walioliitia jina lake; 
walimwita Bwana, 
naye aliwajibu. 
 7 Alizungumza nao kutoka nguzo ya wingu; 
walizishika sheria zake na amri alizowapa. 
 8 Ee Bwana, wetu, 
ndiwe uliyewajibu, 
kwa Israeli ulikuwa Mungu mwenye kusamehe, 
ingawa uliadhibu matendo yao mabaya. 
 9 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu, 
mwabuduni kwenye mlima wake mtakatifu, 
kwa maana Bwana Mungu wetu ni mtakatifu.