Zaburi 101
Ahadi Ya Kuishi Kwa Uadilifu Na Kwa Haki 
Zaburi ya Daudi. 
 1 Nitaimba juu ya upendo wako na haki yako; 
kwako wewe, Ee Bwana, nitaimba sifa. 
 2 Nitazingatia kuishi maisha yasiyo na lawama: 
utakuja kwangu lini? 
Nitatembea nyumbani mwangu 
kwa moyo usio na lawama. 
 3 Sitaweka mbele ya macho yangu 
kitu kiovu. 
Ninayachukia matendo ya watu wasio na imani; 
hawatashikamana nami. 
 4 Moyo wa ukaidi utakuwa mbali nami; 
nitajitenga na kila ubaya. 
 5 Kila amsingiziaye jirani yake kwa siri, 
huyo nitamnyamazisha; 
mwenye macho ya dharau na moyo wa kiburi 
huyo sitamvumilia. 
 6 Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi, 
ili waweze kuishi pamoja nami; 
yeye ambaye moyo wake hauna lawama 
atanitumikia. 
 7 Mdanganyifu hatakaa 
nyumbani mwangu, 
yeye asemaye kwa uongo 
hatasimama mbele yangu. 
 8 Kila asubuhi nitawanyamazisha 
waovu wote katika nchi; 
nitamkatilia mbali kila mtenda mabaya 
kutoka mji wa Bwana.