Zaburi 114
Maajabu Ya Mungu Wakati Israeli Walipotoka Misri 
 1 Wakati Israeli walipotoka Misri, 
nyumba ya Yakobo kutoka kwa watu wa lugha ngeni, 
 2 Yuda alifanywa makao matakatifu ya Mungu, 
Israeli akawa milki yake. 
 3 Bahari ilitazama ikakimbia, 
Yordani ulirudi nyuma, 
 4 milima ilirukaruka kama kondoo dume, 
vilima kama wana-kondoo. 
 5 Ee bahari, ni nini kilichokufanya ukakimbia, 
nawe, ee Yordani, ukarudi nyuma, 
 6 enyi milima mkarukaruka kama kondoo dume, 
enyi vilima, kama wana-kondoo? 
 7 Ee dunia, tetemeka mbele za Bwana, 
mbele za Mungu wa Yakobo, 
 8 aliyegeuza mwamba kuwa dimbwi la maji, 
mwamba mgumu kuwa chemchemi za maji.