Zaburi 113
Kumsifu Bwana Kwa Wema Wake 
 1 Msifuni Bwana. 
Enyi watumishi wa Bwana msifuni, 
lisifuni jina la Bwana. 
 2 Jina la Bwana na lisifiwe, 
sasa na hata milele. 
 3 Kuanzia mawio ya jua hadi machweo yake, 
jina la Bwana linapaswa kusifiwa. 
 4  Bwana ametukuka juu ya mataifa yote, 
utukufu wake juu ya mbingu. 
 5 Ni nani aliye kama Bwana Mungu wetu, 
Yeye ambaye ameketi juu kwenye kiti cha enzi, 
 6 ambaye huinama atazame chini 
aone mbingu na nchi? 
 7 Huwainua maskini kutoka mavumbini, 
na kuwanyanyua wahitaji kutoka kwenye jalala, 
 8 huwaketisha pamoja na wakuu, 
pamoja na wakuu wa watu wake. 
 9 Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake, 
akiwa mama watoto mwenye furaha. 
Msifuni Bwana.