Zaburi 121
Bwana Mlinzi Wetu 
Wimbo wa kwenda juu. 
 1 Nayainua macho yangu nitazame vilima, 
msaada wangu utatoka wapi? 
 2 Msaada wangu hutoka kwa Bwana, 
Muumba wa mbingu na dunia. 
 3 Hatauacha mguu wako uteleze, 
yeye akulindaye hatasinzia, 
 4 hakika, yeye alindaye Israeli 
hatasinzia wala hatalala usingizi. 
 5  Bwana anakulinda, 
Bwana ni uvuli wako mkono wako wa kuume, 
 6 jua halitakudhuru mchana, 
wala mwezi wakati wa usiku. 
 7  Bwana atakukinga na madhara yote, 
atayalinda maisha yako, 
 8  Bwana atakulinda unapoingia na unapotoka, 
tangu sasa na hata milele.