Zaburi 122
Sifa Kwa Yerusalemu 
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi. 
 1 Nilishangilia pamoja na wale walioniambia, 
“Twende nyumbani ya Bwana.” 
 2 Ee Yerusalemu, miguu yetu imesimama 
malangoni mwako. 
 3 Yerusalemu imejengwa vyema kama mji 
ambao umeshikamanishwa pamoja. 
 4 Huko ndiko makabila hukwea, 
makabila ya Bwana, 
kulisifu jina la Bwana kulingana na maagizo 
waliopewa Israeli. 
 5 Huko viti vya enzi vya hukumu hukaa, 
viti vya enzi vya nyumba ya Daudi. 
 6 Omba kwa ajili ya amani ya Yerusalemu: 
“Wote wakupendao na wawe salama. 
 7 Amani na iwepo ndani ya kuta zako 
na usalama ndani ya ngome zako.” 
 8 Kwa ajili ya ndugu zangu na marafiki, 
nitasema, “Amani iwe ndani yako.” 
 9 Kwa ajili ya nyumba ya Bwana Mungu wetu, 
nitatafuta mafanikio yako.