Zaburi 124
Shukrani Kwa Ukombozi Wa Israeli 
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi. 
 1 Kama Bwana asingalikuwa upande wetu; 
Israeli na aseme sasa: 
 2 kama Bwana asingalikuwa upande wetu, 
wakati watu walipotushambulia, 
 3 wakati hasira yao ilipowaka dhidi yetu, 
wangalitumeza tungali hai, 
 4 mafuriko yangalitugharikisha, 
maji mengi yangalitufunika, 
 5 maji yaendayo kasi 
yangalituchukua. 
 6  Bwana asifiwe, 
yeye ambaye hakuruhusu turaruliwe kwa meno yao. 
 7 Tumeponyoka kama ndege 
kutoka mtego wa mwindaji; 
mtego umevunjika, 
nasi tukaokoka. 
 8 Msaada wetu ni katika jina la Bwana, 
Muumba wa mbingu na dunia.