Zaburi 125
Usalama Wa Watu Wa Mungu 
Wimbo wa kwenda juu. 
 1 Wale wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni, 
ambao hauwezi kutikisika, bali wadumu milele. 
 2 Kama milima inavyozunguka Yerusalemu, 
ndivyo Bwana anavyowazunguka watu wake 
sasa na hata milele. 
 3 Fimbo ya waovu haitadumu juu ya nchi 
waliopewa wenye haki, 
ili wenye haki wasije wakatumia 
mikono yao kutenda ubaya. 
 4 Ee Bwana, watendee mema walio wema, 
wale walio wanyofu wa moyo. 
 5 Bali wale wanaogeukia njia zilizopotoka, 
Bwana atawafukuza pamoja na watenda mabaya. 
Amani iwe juu ya Israeli.