Zaburi 126
Kurejezwa Kutoka Utumwani 
Wimbo wa kwenda juu. 
 1  Bwana alipowarejeza mateka Sayuni, 
tulikuwa kama watu walioota ndoto. 
 2 Vinywa vyetu vilijaa kicheko, 
ndimi zetu zilijaa nyimbo za shangwe. 
Ndipo iliposemwa miongoni mwa mataifa, 
“Bwana amewatendea mambo makuu.” 
 3  Bwana ametutendea mambo makuu, 
nasi tumejaa furaha. 
 4 Ee Bwana, turejeshee watu wetu waliotekwa, 
kama vijito katika Negebu. 
 5 Wapandao kwa machozi 
watavuna kwa nyimbo za shangwe. 
 6 Yeye azichukuaye mbegu zake 
kwenda kupanda, huku akilia, 
atarudi kwa nyimbo za shangwe, 
akichukua miganda ya mavuno yake.