Zaburi 127
Bila Mungu, Kazi Ya Mwanadamu Haifai 
Wimbo wa kwenda juu. Wa Solomoni. 
 1  Bwana asipoijenga nyumba, 
wajengao hufanya kazi bure. 
Bwana asipoulinda mji, 
walinzi wakesha bure. 
 2 Mnajisumbua bure kuamka mapema 
na kuchelewa kulala, 
mkitaabikia chakula: 
kwa maana yeye huwapa usingizi wapenzi wake. 
 3 Wana ni urithi utokao kwa Bwana, 
watoto ni zawadi kutoka kwake. 
 4 Kama mishale mikononi mwa shujaa 
ndivyo walivyo wana awazaao mtu katika ujana wake. 
 5 Heri mtu ambaye podo lake 
limejazwa nao. 
Hawataaibishwa wanaposhindana 
na adui zao langoni.