Zaburi 128
Thawabu Ya Kumtii Bwana 
Wimbo wa kwenda juu. 
 1 Heri ni wale wote wamchao Bwana, 
waendao katika njia zake. 
 2 Utakula matunda ya kazi yako; 
baraka na mafanikio vitakuwa vyako. 
 3 Mke wako atakuwa kama mzabibu uzaao 
ndani ya nyumba yako; 
wana wako watakuwa kama machipukizi ya mizeituni 
kuizunguka meza yako. 
 4 Hivyo ndivyo atakavyobarikiwa 
mtu amchaye Bwana. 
 5  Bwana na akubariki kutoka Sayuni 
siku zote za maisha yako, 
na uone mafanikio ya Yerusalemu, 
 6 nawe ujaliwe kuishi uone watoto wa watoto wako. 
Amani iwe juu ya Israeli.