Zaburi 129
Maombi Dhidi Ya Adui Za Israeli 
Wimbo wa kwenda juu. 
 1 Wamenionea mno tangu ujana wangu; 
Israeli na aseme sasa: 
 2 wamenionea mno tangu ujana wangu, 
lakini bado hawajanishinda. 
 3 Wakulima wamelima mgongo wangu, 
na kufanya mifereji yao mirefu. 
 4 Lakini Bwana ni mwenye haki; 
amenifungua toka kamba za waovu. 
 5 Wale wote waichukiao Sayuni 
na warudishwe nyuma kwa aibu. 
 6 Wawe kama majani juu ya paa, 
ambayo hunyauka kabla hayajakua; 
 7 kwa hayo mvunaji hawezi kujaza vitanga vyake, 
wala akusanyaye kujaza mikono yake. 
 8 Wale wapitao karibu na wasiseme, 
“Baraka ya Bwana iwe juu yako; 
tunakubariki katika jina la Bwana.”