Zaburi 130
Kuomba Msaada 
Wimbo wa kwenda juu. 
 1 Kutoka vilindini ninakulilia, Ee Bwana. 
 2 Ee Bwana, sikia sauti yangu. 
Masikio yako na yawe masikivu 
kwa kilio changu unihurumie. 
 3 Kama wewe, Ee Bwana, ungeweka kumbukumbu ya dhambi, 
Ee Bwana, ni nani angeliweza kusimama? 
 4 Lakini kwako kuna msamaha, 
kwa hiyo wewe unaogopwa. 
 5 Namngojea Bwana, nafsi yangu inangojea, 
katika neno lake naweka tumaini langu. 
 6 Nafsi yangu inamngojea Bwana 
kuliko walinzi waingojeavyo asubuhi, 
naam, kuliko walinzi 
waingojeavyo asubuhi. 
 7 Ee Israeli, mtumaini Bwana, 
maana kwa Bwana kuna upendo usiokoma, 
na kwake kuna ukombozi kamili. 
 8 Yeye mwenyewe ataikomboa Israeli 
kutoka dhambi zao zote.