Zaburi 137
Maombolezo Ya Israeli Uhamishoni 
 1 Kando ya mito ya Babeli tuliketi, tukaomboleza 
tulipokumbuka Sayuni. 
 2 Kwenye miti ya huko 
tulitundika vinubi vyetu, 
 3 kwa maana huko hao waliotuteka 
walitaka tuwaimbie nyimbo, 
watesi wetu walidai nyimbo za furaha; 
walisema, “Tuimbieni wimbo mmoja kati ya nyimbo za Sayuni!” 
 4 Tutaimbaje nyimbo za Bwana, 
tukiwa nchi ya kigeni? 
 5 Nikikusahau wewe, ee Yerusalemu, 
basi mkono wangu wa kuume na usahau ujuzi wake. 
 6 Ulimi wangu ushikamane na kaakaa la kinywa changu 
kama sitakukumbuka wewe, 
kama nisipokufikiri Yerusalemu 
kuwa furaha yangu kubwa. 
 7 Kumbuka, Ee Bwana, walichokifanya Waedomu, 
siku ile Yerusalemu ilipoanguka. 
Walisema, “Bomoa, Bomoa 
mpaka kwenye misingi yake!” 
 8 Ee binti Babeli, uliyehukumiwa kuangamizwa, 
heri yeye atakayekulipiza wewe 
kwa yale uliyotutenda sisi: 
 9 yeye ambaye atawakamata watoto wako wachanga 
na kuwaponda juu ya miamba.