Zaburi 138
Maombi Ya Shukrani 
Zaburi ya Daudi. 
 1 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kwa moyo wangu wote, 
mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako. 
 2 Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu, 
nami nitalisifu jina lako 
kwa ajili ya upendo wako 
na uaminifu, 
kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako 
juu ya vitu vyote. 
 3 Nilipoita, ulinijibu; 
ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari. 
 4 Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Bwana, 
wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako. 
 5 Wao na waimbe kuhusu njia za Bwana, 
kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu. 
 6 Ingawa Bwana yuko juu, 
humwangalia mnyonge, 
bali mwenye kiburi 
yeye anamjua kutokea mbali. 
 7 Nijapopita katikati ya shida, 
wewe unayahifadhi maisha yangu, 
unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu, 
kwa mkono wako wa kuume unaniokoa. 
 8  Bwana atatimiza kusudi lake kwangu, 
Ee Bwana, upendo wako wadumu milele: 
usiziache kazi za mikono yako.