Zaburi 141
Maombi Ya Kuhifadhiwa Dhidi Ya Uovu 
Zaburi ya Daudi. 
 1 Ee Bwana, ninakuita wewe, uje kwangu hima. 
Sikia sauti yangu ninapokuita. 
 2 Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba; 
kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni. 
 3 Ee Bwana, weka mlinzi kinywani mwangu, 
weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu. 
 4 Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya, 
nisije nikashiriki katika matendo maovu 
pamoja na watu watendao mabaya, 
wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa. 
 5 Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma; 
na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu. 
Kichwa changu hakitalikataa. 
Hata hivyo, maombi yangu daima 
ni kinyume cha watenda mabaya, 
 6 watawala wao watatupwa chini 
kutoka kwenye majabali, 
waovu watajifunza kwamba maneno yangu 
yalikuwa kweli. 
 7 Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi, 
ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.” 
 8 Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mwenyezi, 
ndani yako nimekimbilia, usiniache nife. 
 9 Niepushe na mitego waliyonitegea, 
kutokana na mitego iliyotegwa na watenda mabaya. 
 10 Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe, 
wakati mimi ninapita salama.