Zaburi 142
Maombi Ya Kuokolewa Dhidi Ya Watesi 
Utenzi wa Daudi. Alipokuwa pangoni. Maombi. 
 1 Namlilia Bwana kwa sauti, 
nainua sauti yangu kwa Bwana anihurumie. 
 2 Namimina malalamiko yangu mbele zake, 
mbele zake naeleza shida zangu. 
 3 Wakati roho yangu inapozimia ndani yangu, 
wewe ndiwe unajua njia zangu. 
Katika njia ninayopita 
watu wameniwekea mtego. 
 4 Tazama kuume kwangu na uone, 
hakuna hata mmoja anayejihusisha nami. 
Sina kimbilio, 
hakuna anayejali maisha yangu. 
 5 Ee Bwana, nakulilia wewe, 
nasema, “Wewe ni kimbilio langu, 
fungu langu katika nchi ya walio hai.” 
 6 Sikiliza kilio changu, 
kwa sababu mimi ni mhitaji sana; 
niokoe na wale wanaonifuatilia, 
kwa kuwa wamenizidi nguvu. 
 7 Nifungue kutoka kifungo changu, 
ili niweze kulisifu jina lako. 
Ndipo wenye haki watanizunguka, 
kwa sababu ya wema wako kwangu.