Zaburi 111
Sifa Za Bwana Kwa Matendo Ya Ajabu 
 1 Msifuni Bwana. 
Nitamtukuza Bwana kwa moyo wangu wote, 
katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko. 
 2 Kazi za Bwana ni kuu, 
wote wanaopendezwa nazo huzitafakari. 
 3 Kazi zake zimejaa fahari na utukufu, 
haki yake hudumu daima. 
 4 Amefanya maajabu yake yakumbukwe, 
Bwana ni mwenye neema na huruma. 
 5 Huwapa chakula wale wanaomcha, 
hulikumbuka agano lake milele. 
 6 Amewaonyesha watu wake uwezo wa kazi zake, 
akiwapa nchi za mataifa mengine. 
 7 Kazi za mikono yake ni za uaminifu na haki, 
mausia yake yote ni ya kuaminika. 
 8 Zinadumu milele na milele, 
zikifanyika kwa uaminifu na unyofu. 
 9 Aliwapa watu wake ukombozi, 
aliamuru agano lake milele: 
jina lake ni takatifu na la kuogopwa. 
 10 Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima, 
wote wanaozifuata amri zake wana busara. 
Sifa zake zadumu milele. 
*^ Zaburi hii imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.